SAKATA YA UZAJI WA MBOLEA GHUSHI NCHINI

Imeratibiwa kuwa, mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali anahitajika kuweka paruanja wote waliohusika na utapeli huu, na kubaini ikiwa au la wasimamizi wa KEBS walipanga njama na watuhumiwa, na pia ikiwa walizembea na kupelekea utepetevu kazini badala ya kuhakikishia wananchi ubora wa bidhaa zozote.

Apr 1, 2024 - 19:45
 0  16
SAKATA YA UZAJI WA MBOLEA GHUSHI NCHINI
picha kwa hisani

Waziri Mkuu Musalia Mudavadi, ametoa kauli yake kuhusu utata unaoligubika swala zima la uwepo wa mbolea ghushi nchini. Kwenye usemi wake, Mudavadi amesema kuwa, “Serikali haiezikuwa inajitahidi kuweka miundo msingi na mipango thabiti kustawisha kilimo kama mojawapo ya Agenda zake, halafu mtu mwenye fikira potovu anaingiza mbolea ghushi kwa madai kuwa anafanya biashara, ilhali anaharibu zile hatua tumepiga.”              

Waziri Mkuu Mudavadi, Picha ni kwahisani

Wasimamizi wakuu wa Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa (KEBS) na pia wale wa Halmashauri ya Nafaka, na Mazao (NCPB) chuma chao ki motoni. Hii ni baada ya wabunge kutaka uchunguzi wa kina kufanywa kutokana na kuwepo kwa mbolea ghushi nchini. Haya yameibuka kutokana shtuma na tetesi miongoni mwa wananchi kuwa wameuziwa mojawapo ya pembejeo muhimu, isiyo hakiki viwango vya ubora hitajika kwenye maeneo mbalimbali nchini. 

Shirika La Kukadiria Ubora wa Bidhaa (KEBS) limelimbikizia lawama mwanabiashara mmoja nchini anayejihusisha na uuzaji wa mbolea, baada ya kubainika kuwa muuzaji huyu alisambazia Halmashauri ya Nafaka, na Mazao (NCPB) mbolea mbovu. 

   

       

Nembo ya NCPB na KEBS mtawalia, picha ni kwa hisani

Kulingana na Kamati ya Bunge la Kitaifa ya Uwekezaji, (Public Investment Committee on Commercial Affairs and Energy), mkaguzi mkuu wa serikali ameagizwa afanye upekuzi ndani ya muda wa mwezi mmoja, ili kutoa mwanga wa ni nani anafaa kuchukuliwa hatua za kisheria. 

Imeratibiwa kuwa, mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali anahitajika kuweka paruanja wote waliohusika na utapeli huu, na kubaini ikiwa au la wasimamizi wa KEBS walipanga njama na watuhumiwa, na pia ikiwa walizembea na kupelekea utepetevu kazini badala ya kuhakikishia wananchi ubora wa bidhaa zozote.

Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni mbunge wa Pokot Kusini Mheshimiwa David Pkosing alisema, “We need to know the batching mechanism for KEBS to ascertain are these people passive that they only give okay to manufacturers and leave it there. Is that the case, if so then we are doomed as Kenyans?”

Ni maswala ambayo yalijitokeza baada ya malalamishi mengi kutoka kwa wananchi, ambayo yaliwasukuma wabunge wanachama wa kamati hii kupendekeza kujiuzulu kwa wasimamizi wakuu wa Shirika la Kukadiria Ubora wa bidhaa ili Kurusu uchunguzi kuendelezwa ifaavyo na wahusika kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria. Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi alisema kuwa, “Ni ufisadi wa hali ya juu. Je,kama KEBS mmependekeza wahusika kuwajibika? Jiuzulu ile kutoa nafasi kwa uchunguzi wa kina kufanywa.”

Wabunge wanataka kuudadavua Mkataba wa Maelewano (MoU) kati ya kampuni moja iitwayo SBL-Innovate Manufacturers Limited na NCPB kukitegua kitendawili kinachozingira uagizaji, usambazaji na uuzaji wa mbolea ghushi nchini, jambo ambalo limewaacha wakulima kwenye njia panda, wasijue la kufanya haswa kwenye msimu huu wa upanzi. Kulingana na wabunge, kuna ukosefu wa uadilifu kwenye KEBS na NCPB, hali ambayo ilirahisisha kuingizwa kwa mbolea feki nchini Kenya na kuhatarisha mfumo ambao serikali imeweka wa kuzalisha chakula kwa wingi ili kukabiliana na mfumko wa bei za vyakula na njaa.

Uchunguzi huu pia unatarajiwa kufichua mchakato ambao ulitumiwa na KEBS kuagiza kurejeshwa kwa mbolea hiyo ambayo ilikuwa ishasambazwa na NCPB na kasha kurudishwa kwenye maghala yake. 

Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa KEBS Bi Esther Gitari amewaambia wabunge kuwa swala hilo linachunguzwa kikamilifu na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka wa Umma ambaye atapendekeza hatua zaidi kuchukuliwa dhidi ya wahusika. “Tumemwandikia Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma kuhusu swala hili, na tumepeana stakabadhi zote kutokana na uchunguzi wetu wa awali”, Gitari alisema.

Hata hivo, wabunge hawajafurahishwa na hatua ya serikali kutowachukulia hatua wahusika, kwani hadi sasa hawajatiwa mbaroni ili kufikishwa kwenye mahakama kujibu mashtaka. Hii ni baada ya kashfa hii kuibuliwa na KEBS siku kadhaa zilizopita. “Kwa nini mtu aliyehusishwa na kashfa hii hajatiwa mbaroni. Hamna mbinu kama nchi ya kumkamata? Anafaa kuwa korokoroni au mbinguni,” Pkosing alisema.

La kustaajabisha ni kuwa, kulingana na stakabadhi za KEBS zilizoko mbele ya kamati ya bunge, imedhihirika kuwa SBL-Innovate Manufacturer Limited imekuwa ikisambaza mbolea iliyo chini ya viwango vya ubora hitajika kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja sasa bila kugunduliwa. Kulingana na KEBS, kampuni hii ilituma ombi la kupata kusajiliwa mnamo Januari 3, 2023, and ombi lao likapata jibu chanya Januari 28, mwaka uo huo wa 2023.

Shirika la KEBS liliidhinisha kampuni ya SBL-Innovate Manufacturer kusambaza mbolea ya kikaboni, ila kampuni hiyo ikasambaza mbolea ya diatomite, ambayo hutengenezwa kwa njia za kibayolojia kutokana na Silica ili kuukuza udongo. Kwa muda sasa, wakulima wamekuwa wakipanga foleni ndefu kununua bidhaa ambayo sio bora, lakini iliyo na nembo ya KEBS.  

Shirika la KEBS limeashiria kuanzisha upekuzi na msako kutokana kufuatia dokezo kutoka kwa wananchi, na kuwa kufikia sasa, magunia 5, 840 yamenaswa na kurejeshwa kutokana na msako huo.

Ni swala ambalo tutazidi tutalifuatilia kwa karibu mno ili kujua ni hatua gani zitachukuliwa dhidi ya wahusika, wakati ambapo hata viongozi mbalimbali wa kidini wamekashifu kwa ukali, na kutaka serikali kuwachukulia hatua wahusika kwenye kashfa hii. Kila mwanachi anataka kujua mwelekeo upi serikali itachukua kuziba mianya kama hii na kuuzima utepetevu wa maofisa wa serikali kwenye sekta ainati.

 

What's Your Reaction?

like

dislike

love

funny

angry

sad

wow